Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imewashukia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ikisema wanatumia vibaya mamlaka waliyopewa kwa kuamrisha watumishi wa umma kuwekwa ndani kwa makosa yasiyostahili adhabu hiyo.
Akisoma taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2016/17, mjumbe wa kamati Ester Mahawe alisema, “Ipo mifano kadhaa ikiwa ni pamoja na mkuu wa mkoa mmojawapo nchini aliamuru daktari wa mkoa wake awekwe rumande kwa sababu hakutangaza kuwapo kwa ugonjwa wa kipindupindu.”
Bila kutaja majina, alitoa mfano mwingine wa mkuu wa wilaya moja ya Mkoa wa Dar es Salaam aliyeamuru watumishi waliochelewa kazini wawekwe ndani na mwingine wa Mkoa wa Arusha aliyeamuru mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni nchini awekwe ndani kwa kuandika habari kuhusu kero ya ukosefu wa maji, ambayo mkuu huyo wa wilaya alitafsiri kuwa ni uchochezi.
Mahawe alitoa mfano mwingine kuwa ni mkurugenzi wa halmashauri aliyeamuru mwalimu wa sekondari kudeki darasa mbele ya wanafunzi kwa sababu ni chafu.
“Mkuu wa mkoa kutumia lugha zisizofaa kwa watumishi kuwa ni wezi, wajinga wasiokuwa na akili timamu, hawa ndio vichaa tunaohangaika nao ni kudhalilisha utu wa mtu na kuvunja misingi ya Katiba,” alisema.
Alitoa ufafanuzi akisema Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 sura ya 97 imeweka masharti muhimu kwa mkuu wa mkoa na wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya kuamrisha mtu akamatwe.
“Vifungu hivyo vinaeleza kwamba, itafanya hivyo pale tu ambako atakuwa amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika athari yake huwa ni kukamatwa na kushtakiwa,” alisema.
Alitaka viongozi wote na wabunge kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na utaratibu uliopo na kwamba, kinyume na hapo watakuwa wameshindwa kutimiza wajibu wa kuwa mfano kwa wanaowaongoza.
Mbali na kamati, wabunge waliochangia mjadala wa taarifa hiyo walisema mambo yanayofanyika ni matumizi mabaya ya madaraka ya mamlaka waliyopewa.
Mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia alisema watendaji wa Serikali wanashindwa kuelewa kauli zinazotolewa na Rais, jambo linalowafanya watekeleze maagizo tofauti na dhamira yake.
Mtulia, akitoa mfano wa kauli ya kutaka vyombo vya usafiri vitakavyopita katika barabara za mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam kung’olewa matairi, alisema watendaji hawakumwelewa Rais kuwa alikuwa akimaanisha wachukuliwe hatua za kisheria.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni kwa utaratibu alioufanya baada ya wilaya yake kutofanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha nne ya mwaka jana.
“Naomba tumpongeze DC wa Kigamboni (Hashim Mgandilwa) kwa hatua aliyoichukua ya kuitisha kikao cha idara husika na kuwapa nafasi ya kufanya utafiti kabla ya kuchukua hatua,” alisema Waitara.
Hata hivyo, aliwashutumu wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Simiyu kwa kuwaweka ndani na kuwadhalilisha watendaji wanaokwenda kinyume na wanachotaka.
Mbunge wa Muheza (CCM), Adadi Rajab alisema dhana ya madaraka kwa baadhi ya viongozi inakwenda vibaya na kwamba kuna haja ya kupata elimu.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alitaka Serikali kujenga uwezo wa taasisi badala ya kutegemea mtu ili kipindi chake cha uongozi kitakapopita taasisi iendelee.
Friday, February 3, 2017
Wabunge wawajia juu wakuu wa Mikoa,Wilaya
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
New Posts
IJUE SCANIA P380[Mende]
Scania P380 Mende ni nini? Scania P380 ni mojawapo ya malori maarufu yaliyoundwa kwa nguvu na ufanisi wa hali ya juu, hasa kwa mazingira ya ...
-
Serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura ya mwaka mzima kwa shabaha ya kuzuia kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokuumbw...
-
Wizara ya Ulinzi ya Taiwan imesema leo Jumatatu kuwa imenasa ndege 103 za kivita za China karibu na kisiwa hicho katika muda wa saa 24, ida...
-
Askari wa kike kutoka nchini Tanzania wameshiriki mkutano wa mwaka 2023 wa mtandao wa polisi wanawake duniani (IAWP) nchini New Zealand. Mk...
No comments:
Post a Comment