Anne Kilango
Dar es Salaam. Hatua ya Rais John Magufuli kumteua Anne Kilango Malecela kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano imezua mjadala katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wadau wa siasa, sheria na jinsia huku wengine wakimpongeza.
Uteuzi wa Kilango, ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, umekuja siku chache baada ya aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa na Naibu Waziri, Dk Abdallah Possi kujiuzulu kwenye nafasi hiyo baada ya kuteuliwa kuwa balozi.
Hatua hiyo huenda ilitokana na kitendo cha Rais Magufuli kuwateua Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa wabunge, hali iliyozua minong’ono kuwa amekwenda kinyume na Katiba inayomtaka kuteua walau wabunge watano wanawake katika nafasi zake 10 za uteuzi.
Miongoni mwa mijadala iliyoibuka katika mitandao ya kijamii katika uteuzi wa Kilango ni hatua ya Rais Magufuli kumteua tena baada ya uteuzi wa kwanza wa ukuu wa Mkoa wa Shinyanga ambao aliutengua ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, kwa kutosema ukweli kuhusu taarifa za wafanyakazi hewa.
Akizungumzia hatua ya kutengua uteuzi wa Kilango Aprili mwaka jana, Rais Magufuli alionyesha kusikitishwa na kupewa taarifa ambazo hazikuwa sahihi.
“Nimejiuliza sana, nikajiuliza sana na ni kweli nimejiuliza maswali mengi kwa masikitiko makubwa. Kwa nini mkuu wa mkoa amezungumza kuwa hakukuwa na mtumishi hewa na hakukuwa na adhabu yoyote? Lengo lake lilikuwa nini? Je, kama ni RAS aliyemdanganya, kwa nini alikubali kudanganywa naye akasema uongo? Ni shetani gani aliyemgusa mpaka akaamua kusema uongo?
“Ninasema kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu mpaka jana walishapatikana watumishi hewa 45 na nina uhakika wataongezeka.
“Nasema kwa masikitiko sana, nimeamua nitengue uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, atapangiwa kazi nyingine aliyo na uwezo nayo; na kwa masikitiko hayo hayo nimeamua kutengua uteuzi wa RAS wa Shinyanga kwa sababu inawezekana alimdanganya Mkuu wa Mkoa…” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo swali hilo limejibiwa na kauli ya Rais Magufuli aliyesema atapangiwa kazi nyingine aliyo na uwezo nayo.
Siyo mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuwarejesha watendaji wa Serikali aliowawajibisha na kuahidi kuwapangia kazi nyingine.
Mbali na Kilango, wengine walioondolewa nafasi zao za awali na kupangiwa kazi nyingine ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Yunus Mgaya ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dk Mwele Malecela kuondolewa.
Mwingine aliyetenguliwa Oktoba 29, 2016 ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Diwani Athumani, lakini Novemba 18, 2016 aliteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.
Uteuzi wa Diwani ulitenguliwa muda mfupi baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House), kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili inayofanywa na Kikosi Kazi kilichoundwa na wizara hiyo ambapo alishuhudia pembe 50 zilizokamatwa ndani ya siku mbili.
Hoja ya nyingine katika mjadala huo ni kuhusu kuzingatiwa kwa jinsia katika uteuzi wa nafasi 10 za wabunge na teuzi nyingine katika nafasi za uongozi ndani ya Serikali.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Profesa Ruth Meena alisema tangu mwanzo utawala wa sasa haujatoa kipaumbele kwa wanawake katika nafasi za uteuzi.
“Mimi sitaki kuzungumzia uteuzi wa Anne Kilango, nazungumzia teuzi kwa ujumla. Rais Magufuli aliahidi kwenye kampeni zake mwaka 2015 kuwa hatawaangusha wanawake. Tena kwa takwimu za uchaguzi ule ilionekana walipiga kura wengi, lakini hajaonyesha utashi wa kuteua wanawake tangu mwanzo,” alisema Profesa Meena na kuongeza:
“Ni kinyume kabisa na mikataba ya kimataifa tuliyosaini na ahadi alizotoa kwenye kampeni. Sisi kama wanaharakati tutaendelea kupigania haki hiyo ya wanawake katika uongozi,” aliongeza Profesa Meena.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sophia Simba alisema Rais Magufuli amezingatia wanawake katika teuzi zake.
“Mimi nimefurahia uteuzi wa Mama Anne Kilango…watu wanasema Rais hajazingatia jinsia katika teuzi zake, mimi naona wanawake wengi amewachagua katika nafasi zake,” alisema Simba.
Akizungumzia uteuzi huo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema uko sahihi na ni utekelezaji wa Katiba.
“Uteuzi wa Mama Kilango ni sahihi. Sina pingamizi nao. Siyo hivyo tu, tunatarajia na nafasi mbili zilizobaki baada ya Dk Possi kujiuzulu na Spika wa Bunge kupokea barua yake watachaguliwa wanawake. Hilo ni takwa la kikatiba,” alisema Mdee.
Kuhusu hatua ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake kama Mkuu wa Mkoa, Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), alisema halikuwa kosa kubwa la kutenguliwa.
“Kwa mtazamo wangu, suala la kutotoa ‘takwimu’ sahihi pekee, tena Mara ‘moja tu’ hakiwezi kuwa kigezo cha kumfukuza mtu kazi. Mama Kilango ndiyo alikuwa ameripoti kituo cha kazi na yeye kama alivyo Rais analetewa taarifa na wasaidizi wake ndani ya mkoa, wakurugenzi, RAS, DAS, maofisa utumishi na wengineo,” alisema.
Akizungumzia uteuzi huo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mohamed Bakari alisema kuna maswali mengi yameibuka.
“Mtu aliondolewa kwa kutoa taarifa za uongo, leo tena anateuliwa kuwa mbunge, ni nafasi kubwa ambayo hata wakuu wa mikoa wanaitamani,” alisema.
Anne Kilango azungumza
Akizungumzia uteuzi huo Kilango alisema kila jambo hutokea kwa makusudi ya Mungu.
“Nilijua kabisa Mungu ana sababu ya kuniweka katika nafasi ile (ukuu wa mkoa wa Shinyanga) kwa siku 28 tu,” alisema Mbunge huyo wa zamani wa Same Mashariki.
Alisema anaamini Mungu alimtoa katika nafasi hiyo ya ukuu wa mkoa kwa sababu alimpangia kitu kingine kizuri zaidi.
“Baada ya kutenguliwa sikusikitika bali niliendelea na biashara zangu na shughuli nyingine za chama,” alisema alipozungumza na kituo cha televisheni cha Azam.
JIUNGE NASI KATIKA
INSTA
GRAM @Officialobby
FACEBOOK @Officialobby
YOUTUBE @Officialobby
No comments:
Post a Comment