Na. Tundu Lissu
Waheshimiwa na makamanda poleni kwa mapambano na hongereni kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi hizi. Naona kila mmoja wetu anasikitika jinsi matokeo ambavyo yamekuwa tofauti na matarajio yetu na kazi tuliyoifanya.
Ni rahisi, katika mazingira haya ya kushindwa na kabla vumbi halijaisha, kuanza kulalamika, kunyoosheana vidole na kukatishana tamaa. Hii haitusaidii sana. Badala yake, tunachohitaji zaidi ni ‘brainstorming’ kuliko ‘blamestorming.’ Naomba nifanye ya kwanza. Chaguzi ndogo za ubunge au udiwani ni ngumu sana kushinda katika mazingira halisi ya nchi yetu.
Mifano michache inathibitisha ukweli huu. Katika election cycle ya ’05-’10, tulishinda Jimbo la Tarime lakini tukapigwa Biharamulo Magharibi na Busanda. Tarime lilikuwa Jimbo letu tangu Uchaguzi Mkuu wa ’05, Busanda lilikuwa la maCCM na Biharamulo Magharibi lilikuwa la TLP.
Sikumbuki vizuri kama tulishinda Kata hata moja katika mzunguko wa uchaguzi wa kipindi hicho.
Katika election cycle ya ’10-’15, tulipigwa Igunga licha ya kazi kubwa tuliyofanya, lakini tukashinda Arumeru Mashariki iliyokuwa chini ya maCCM. Vile vile tulishindwa Kalenga, Chalinze na Ulanga Magharibi yaliyokuwa ya maCCM tangu Uchaguzi Mkuu wa ’10.
Kwenye chaguzi za Kata za ’12 kama mnakumbuka, licha ya kazi kubwa na rasilimali nyingi, tulipata Kata tatu tu kati ya 26 zilizokuwa zinagombaniwa. Ukiachia Ifakara Mjini ya Mh. Juakali, Kata nyingine mbili – Kiboriloni na Iseke – zilikuwa zetu tangu Uchaguzi Mkuu wa ’10.
Kwa mantiki hii, matokeo ya jana sio ya kushangaza sana. Kata ya Duru ilikuwa ya kwetu na tumeitetea, nyingine zote tulikopigwa zilikuwa za maCCM. Hatujanyang’anywa iliyokuwa yetu, hatujanyakua zilizokuwa zao. Hata hivyo, funzo kubwa zaidi la historia ya chaguzi hizi ni hili hapa: licha ya kupigwa kwenye chaguzi ndogo hizi, tumeendelea kufanya vizuri zaidi katika kila Uchaguzi Mkuu uliofuatia kipigo cha chaguzi ndogo.
Mwaka ’10 tulifanya vizuri zaidi licha ya kupigwa Busanda na Biharamulo Magharibi katika mzunguko wa ’05-’10. In fact, tulichukua Jimbo la Biharamulo Magharibi mwaka huo. Na tulipata Kata nyingi zaidi ’10 kuliko ilivyokuwa ’05. Mwaka ’15 tulipata ushindi mkubwa zaidi katika Kata na majimbo licha ya kupigwa kwenye chaguzi ndogo za mzunguko wa ’10-’15.
Hoja yangu hapa ni kwamba uchaguzi wa marudio hauna direct and negative bearing kwenye matokeo yetu ya Uchaguzi Mkuu unaofuatia. On the contrary, uchaguzi wa marudio unatupa fursa ya kupanda mbegu ambayo, ikitunzwa vizuri, inakuwa na mazao bora kwenye chaguzi zinazofuatia.
Kwa upande mwingine, chaguzi za marudio – kwa sababu ya udogo au uchache wa maeneo yanayogombaniwa – yanawapa maCCM fursa ya kutumia nguvu kubwa za rasilimali na za kidola ukilinganisha na tunazotumia sisi. Kwenye Uchaguzi Mkuu unaofuatia, nguvu hizo zinasambazwa nchi nzima na kwa hiyo effectiveness yake inapungua.
Ndio maana tumefanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu kuliko kwenye chaguzi ndogo za marudio. Hili, kwa maoni yangu, ndilo fundisho kuu la chaguzi hizi za marudio. Hatuna sababu kubwa ya kushangilia kutokana na matokeo ya jana. Hata hivyo, hatuna sababu yoyote ya kuomboleza pia. Obviously, maCCM na wapambe wao wataandika ‘wasifu wa marehemu’ wa CHADEMA/UKAWA na kuutangaza dunia nzima na kwa sauti kubwa. Hilo lisitupofushe macho yetu, hata kama linakera sana.
Tutathmini kazi tuliyoifanya na matokeo tuliyoyapata. Tupate mafundisho sahihi ya kazi hiyo na matokeo yake. Tutumie mafundisho hayo kwa kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya ‘the real prize’: 2020.
No comments:
Post a Comment