Makao makuu ya Tanesco jijini Dar es Salaam
KAIMU Mkurugenzi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka ameahidi kuongeza ufanisi wa shirika katika kuzalisha umeme sambamba kudhibiti upotevu wa umeme na mapato. Aidha, amepanga kupambana na wezi wa umeme na vishoka ambao wamekuwa wakiliibia shirika hilo, jambo ambalo linapunguza mapato ya shirika.
Mwinuka aliyasema hayo kwenye mahojiano, yaliyolenga kuangalia vipaumbele vyake mara baada ya kukabidhiwa wadhifa wa kuliongoza shirika hilo. Mwinuka ambaye alikuwa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha UDSM, aliteuliwa kushika wadhaifa huo, baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Felchesmi Mramba.
Akitaja baadhi ya vipaumbe vyake, Mwinuka ikiwa ni pamoja na upanuzi wa uwezo wa shirika wa kuzalisha umeme, lengo likiwa ni kuzalisha umeme wa ziada, ambao utaweza kuwavutia wawekezaji hususani sekta ya viwanda. “Sisi zao letu ni umeme, itakuwa vizuri katika miaka mingi inayokuja tukahakikisha tunakuwa na umeme wa kutosha. Tusipoweza kupanua uwezo wa kuzalisha umeme, itafika wakati tutashindwa kuongeza kiwanda wala kumuunganishia mteja yeyote.
“Tutakuwa na mikakati ya muda mfupi, kati na muda mrefu, hili ni suala endelevu. Ingawa kwa sasa mahitaji na uwezo wa shirika wa kuzalisha umeme haupishani sana, lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na uwezo wa kuzalisha ziada wa zaidi ya megawati 600, unaweza kumwambia mwekezaji unaweza kuzalisha umeme wa ziada."
Kuhusu suala la miundombinu, Mwinuka alisema atahakikisha miundombinu kama mitambo, mabwawa na njia za kusafirishia umeme, zinakuwa na ubora na uwezo ili kuongeza ufanisi wa huduma. “Katika miundombinu ambayo tunayo, kwa maana ya mitambo tulionayo ya kuzalisha umeme, mabwawa na njia za kusafirishia inatakiwa kuwa bora na yenye uwezo, ili isije ikaporomoka."
No comments:
Post a Comment