Friday, January 6, 2017

Madereva ‘wanyongwa’ na Trafiki kwenye faini

WAKATI Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani likiendelea na operesheni zake, ikiwamo ya kukamata madereva wa magari na pikipiki wanaovunja sheria na kuwatoza faini za papo kwa hapo, imebainika kuwapo dhuluma katika faini hizo.

Jana kupitia mitandao ya kijamii, Jeshi hilo lilianisha makosa ya barabarani yapatayo 20 na adhabu zao ikiwa ni faini na vifungo jela, huku katika baadhi ya makosa, faini zilizoainishwa zikitofautiana na zinazotozwa barabarani.

Adhabu zilizoanishwa ni faini za kati ya Sh 10,000 hadi Sh 50,000 na kifungo cha kati ya miezi sita hadi miaka miwili au vyote kwa pamoja kwa kosa.

Hata hivyo, mbali ya adhabu hizo kuanishwa kwa makosa ya barabarani, askari wa barabarani wamekuwa wakitoza faini isiyopungua Sh 30,000 madereva kwa makosa hata yasiyostahili kutozwa, na hivyo kuzua maswali mengi. 

Licha ya hali hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga aliyezungumza jana na JAMBO LEO alikiri viwango vya adhabu hizo kutolewa, lakini akasema taarifa hiyo inakanganya wananchi akisema wanatoa tafsiri tofauti huku akieleza kwamba, wapo katika mchakato wa kutoa mchanganuo mwingine.

“Hizi ni adhabu za mahakamani, endapo mtu atapelekwa mahakamani, ndiyo maana utaona na vifungu vimeainishwa lakini kwa makosa ya papo kwa hapo ni Sh 30,000 kwa kosa,” alisema.

Baadhi ya madereva waliozungumza na gazeti hili walishangazwa na viwango vya faini wanavyotozwa barabarani wakati sheria ikiweka wazi adhabu husika.

“Mfano ukisahau leseni sheria inataka ulipe faini ya Sh 10,000 lakini tunatozwa Sh 30,000, hii si dhuluma? Naona madereva tunadhulumiwa,” alisema Shabani Ally dereva wa daladala la Buguruni-Chanika.

Joel Ndundu dereva wa bodaboda, Upanga alisema: “Faini tunazotozwa hazilingani na uhalisia bali trafiki hujiamulia, sijui wanapata asilimia 10?”

Makosa 20

Katika mchanganuo huo, mtu akiendesha gari amelewa au kuathiriwa na dawa za kulevya kwa zaidi ya kiwango cha asilimia 0.80 adhabu yake ni faini ya kati ya Sh 15,000 na Sh 50,000 huku adhabu nyingine zikiwa ni kifungo kati ya miaka miwili hadi mitano jela.

Kosa la kutofuata alama za barabarani, ikiwa ni pamoja na taa za barabarani na sehemu wanayovuka waenda kwa miguu, faini ni kati ya Sh 15,000 hadi Sh 30,000 au kifungo cha miezi sita jela au vyote pamoja.

Kuendesha gari kwa kasi isiyoruhusiwa katika eneo husika, adhabu ni faini ya Sh 15,000 hadi Sh 50,000 au kifungo cha miaka miwili na kisichozidi mitano.

Inafafanua kuwa dereva akisahau leseni ya udereva, faini ni Sh 15,000 au kifungo cha miezi sita au vyote pamoja, kutojua leseni iliko faini ni  Sh 20,000 hadi Sh 50,000 au kifungo cha miezi sita jela au vyote.

Kosa la kutumia leseni iliyokwisha muda wake, faini ni Sh 15,000 hadi Sh 30,000 au kwenda jela miezi sita, kutokuwa na bima ya gari na usajili faini ni Sh 15,000 hadi Sh 50,000 au kifungo cha miaka mitano jela.

Dereva kutofunga mkanda faini ni Sh 15,000 au jela miezi sita, abiria aliyekaa mbele bila kufunga mkanda faini ni Sh 30,000 au jela miezi sita au vyote huku abiria wa nyuma asiyefunga mkanda sheria iko kimya.

Ilieleza kuwa gari ikibainika kuwa na kasoro, faini yake ni Sh 30,000 au jela miezi sita au vyote, kutokuwa na kibao cha pembe tatu faini ni Sh 30,000 hadi Sh 50,000 au jela miezi sita au vyote, kutokuwa na kasha la huduma ya kwanza, faini  ni Sh 30,000 hadi Sh 50,000 au jela miezi sita au vyote.

Aidha, ilibainisha kuwa kukosa kifaa cha kuzimia moto faini ni Sh 30,000 hadi Sh 50,000 au kwenda jela miezi sita au vyote, kutumia simu ya mkononi na kuendesha gari faini ni kati ya Sh 15,000 na Sh 50,000 na kifungo cha kati ya miaka miwili hadi mitano.

Hata hivyo suala la kizimamoto limekuwa na utata, kwani mmiliki wa gari anapokwenda Mamlaka ya Mapato (TRA) kulipia leseni ya barabarani, hulazimika kuongeza Sh 30,000 ambazo zinaonesha ni kwa ajili ya kifaa hicho.

Lakini hata baada ya malipo, mmiliki wa gari hutakiwa tena kwenda Idara ya Zimamoto na Uokoaji, kukinunua kwa bei hiyo hiyo ambayo alishailipia TRA na hivyo malipo kufanyika marambili na kuonekana ni dhuluma pia.

Kwa kosa la kuuzuia askari wa usalama barabarani kufanya shughuli zao,  faini ni Sh 10,000 hadi Sh 20,000 au jela miezi 12 au kutozidi miaka mitano.

Kwa wanaoendesha pikipiki bila kofia ngumu faini ni Sh 15,000 hadi Sh 30,000 au jela miezi sita au vyote, lakini sheria ikiwa haisemi lolote kwa abiria asiyevaa kofia hiyo.

Kujaribu kupita gari la mbele sehemu isiyoruhusiwa faini ni Sh 10,000 au jela miezi sita au vyote na kupita gari kushoto faini ni Sh 20,000 au jela miezi sita au vyote.

No comments:

Post a Comment

New Posts

Libya yatangaza hali ya dharura ya mwaka mzima baada ya mafuriko

  Serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura ya mwaka mzima kwa shabaha ya kuzuia kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokuumbw...