Monday, September 18, 2023

Libya yatangaza hali ya dharura ya mwaka mzima baada ya mafuriko

 


Serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura ya mwaka mzima kwa shabaha ya kuzuia kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokuumbwa na mafuriko makubwa ya mashariki mwa nchi hiyo.


Jumapili iliyopita, kimbunga cha “Daniel” kilipiga maeneo kadhaa mashariki mwa Libya, na hasa hasa miji ya Benghazi, Al-Bayda, Marj, Susa, Shahatt na Derna.


Baada ya kimbunga hicho, Shirika la Afya Duniani lilionya kuhusu kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokumbwa na kimbunga na mafuriko hayo.


Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Haidar al-Sayeh, mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Magonjwa nchini Libya, alitoa taarifa na kutangaza idadi ya sumu ambazo zimeripotiwa kutokana na matumizi ya maji ya kunywa huko Derna, Libya.


Akizungumzia kutotumika maji ya kunywa katika jiji la Derna, Al-Sayeh amesema kuwa, hali ya hatari ya mwaka mmoja itatangazwa katika maeneo yaliyoathiriwa na dhoruba na mafuriko mashariki mwa Libya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wowote wa kuambukiza katika maeneo haya.


Shirika la Afya Duniani lilitangaza siku ya Jumamosi kuwa, zaidi ya watu 9,000 wametoweka katika mji wa Derna mashariki mwa Libya.


Idadi ya waliofariki kutokana na kimbunga hicho nchini Libya hadi sasa imetangazwa kuwa zaidi ya 11,000.

Taiwan yanasa ndege 103 za kivita za China kwenye anga yake



 Wizara ya Ulinzi ya Taiwan imesema leo Jumatatu kuwa imenasa ndege 103 za kivita za China karibu na kisiwa hicho katika muda wa saa 24, idadi kubwa isiyo kawaida.


Kati ya Septemba 17 na 18 asubuhi, Wizara ya Ulinzi imenasa jumla ya ndege 103 za China, ikiwa ni rekodi katika kipindi cha hivi karibuni na inaleta matatizo makubwa ya usalama katika pande zote za mlango wa bahari wa Taiwan na katika kanda,” wizara imesema katika taarifa yake.


“Uchochezi wa kijeshi unaoendelea” kutoka Uchina “unaweza kusababisha kuongezeka kwa mvutano na kuzorota kwa usalama katika eneo hilo,” imeonya wizara hiyo, ambayo inaitaka Beijing “kukomesha mara moja vitendo hivi vya uharibifu vya upande mmoja.”


Kati ya idadi ya ndege za kijeshi zilizonaswa, 40 zilivuka mstari wa wastani – mpaka usio rasmi kati ya China na Taiwan ambao China haitambui – na kuingia katika zili katika eneo la utambulisho wa ulinzi wa anga wa kusini (Adiz) -magharibi na kusini mashariki, kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari. Meli tisa za kivita za China pia zilionekana karibu na kisiwa hicho

Askari wa kike Tanzania washiriki mkutano wa mwaka 2023 New Zealand

 Askari wa kike kutoka nchini Tanzania wameshiriki mkutano wa mwaka 2023 wa mtandao wa polisi wanawake duniani (IAWP) nchini New Zealand.



Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo” Refresh, Renew,Refocus umefunguliwa September 17,2023 mji wa Auckland.





Aidha Mkutano huo umeudhuriwa na mataifa 65 yakiwemo mataifa mengine kutoka Afrika kama vile Tanzania,Ghana na Africa Kusini.





Itakumbukwa mwishoni mwa mwezi Julai Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano kama huo kwa ukanda ya Afrika uliyofanyika jijini Dar es salaam na kuleta matokeo makubwa ya kiutendaji kwa maafisa na askari wa kike ambao walishiriki na mada mbalimbali kufundishwa lengo likiwa kuwaongezea uwezo na maarifa ya kiutendaji.





Mkutano huo uliofunguliwa leo septemba 17,2023 katika mji Auckland Nchini New zealand unaoambatana na mafunzo ya kuwajengea uwezo askari wa kike, sambamba na kutoa fursa na kutengeneza mtandao wa mawasiliano kwa wasimamizi wa sheria.





Mbali na hilo Ujumbe huo kutoka Tanzania uliongozwa na Kamishna wa Polisi CP Suzan Kaganda wa kamisheni ya Utawala na rasilimali watu umetumia mkutano huo kutangaza utalii na vivutio vya kitamaduni vilivyopo Tanzania.



Mkutano huo hutahitimishwa Septemba 21,Mwaka huu.



Urusi yazuia mashambulizi mapya ya ndege zisizo na rubani za Ukraine

 


Urusi imedai kuangusha ndege kadhaa zisizo na rubani za Ukraine katika eneo lililokaliwa la Crimea, katika mkoa wa Moscow pamoja na ile ya Belgorod na Voronezh, karibu na Ukraine.


Ndege kadhaa ziliharibiwa katika eneo lililounganishwa la Crimea, katika mkoa wa Moscow na ile ya Belgorod na Voronezh, usiku wa Jumapili kuamkia leo Jumatatu.


“Drones zilinaswa juu ya maeneo ya magharibi, kusini-magharibi, kaskazini-magharibi na mashariki mwa peninsula ya Crimea, Istra (magharibi) na Domodedovo (kusini) wilaya za mkoa wa Moscow, mikoa ya Belgorod na Voronezh (kusini-magharibi),” Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kwenye Telegramu, bila kubainisha idadi ya ndege zilizoharibiwa au kuripoti uharibifu au majeruhi kufikia hatua hii.


“Vituo vya uzalishaji wa kiwanda cha kivita cha Kharkiv, ambapo ukarabati na utunzaji wa magari ya kivita ya Kikosi cha Wanajeshi wa Ukraine ulikuw ukifanyika, vlipigwa na mashambulizi haya anga,” chanzo hicho pia kimetangaza.


Hapo awali, mkuu wa utawala wa jeshi la Ukraine, Oleg Synegubov, aliripoti kwenye Telegram kwamba moja ya makampuni katika jiji hilo ilipigwa na “makombora manne ya S-300” na moto ukazuka.

WATAKAO TUPA TAKA HOVYO NJOMBE MJINI KUCHUKULIWA HATUA KALI


Katika kuadhimisha siku ya Usafishaji Duniani Septemba 16,2023, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Ndugu Kuruthum Sadick amesema Halmashauri haitamvumilia mwananchi yeyote, atakayeonekana kuchafua mazingira kwa kutupa taka hovyo mitaani na kwenye maeneo yasiyo rasmi.


Akielezea umuhimu wa usafi na kutunza mazingira Mkurugenzi Kuruthum amesema kuwa, usafi ni afya na ukitunza mazingira yanakutunza hivyo kila mwananchi anawajibu wakuhakikisha anafanya usafi kwenye maeneo yanayomzunguka kutunza maeneo ya mabonde na vyanzo vya maji kwa kuacha kutupa takataka hovyo.


Akiwa eneo la bonde linalopita mtaa wa National Housing kata ya Njombe Mjini ,ametoa onyo kwa wananchi ambao wanatupa taka kwenye bonde hilo ambalo siyo dampo rasmi kwa ajili ya takataka nakusema Halmashauri imetenga eneo rasmi kwa ajili ya kutupa taka hivyo bonde hilo lisitumike kutupia taka.


“Tumeweza kujumuika kufanya usafi kwenye hili bonde ni wasihi wananchi kuacha kutupa taka kwenye bonde hili na yeyote atakayebainika hatua kali zitachukuliwa,na tufahamu kuwa kuna vyanzo vyanzo vya maji kwenye bonde hili na tunaelekea msimu wa mvua siyo afya kwa vyanzo vyetu vya maji maana maji haya yanatumika, Halmashauri ina magari yakukusanya taka kupeleka dampo tuache kabisa kutupa taka kwenye eneo hili ambalo siyo rasmi ”


Katika hatua nyingine amesema ili kuhakisha Mji wa Njombe unaendelea kubaki katika hali ya usafi ,Halmashauri ya Mji Njombe itaendelea kuhamasisha na kushiriki usafi wa pamoja kila mwezi ili kuwa kumbusha wananchi kuwa wanawajibu wakutunza mazingira na kufanya usafi mpaka kwenye maeneo yanayowazunguka majumbani.


“Usafi usiishie hapa tu,tufanye usafi hadi majumbani, hii itatukinga na magonjwa, kama kipindupindu”


Kwa upande wake Afisa Afya wa Mkoa wa Njombe Bi.Saada Milanzi amesema ili kuendelea kutunza mazingira Halmashauri zote za mkoa wa Njombe ziendelee kutumia sheria ndogo zilizopitishwa ili kuwawajibisha na kudhibiti utupaji taka kwenye maeneo yasiyo rasmi.


Aidha ametoa wito kwa wananchi kuitikia wito wakushishiriki shughuli za usafi na kutii sheria mbalimbali za usafi na utunzaji wa mazingira zilizowekwa na Halmashauri ili kuweka mazingira safi na kuzuia magonjwa ya mlipuko .


Naye mtendaji wa kata ya Njombe Mjini Enos Lupimo ameeleza mikakati waliyonayo katika kuweka eneo la Mji safi pamoja na kupambana na utupaji wa taka hovyo kwenye maeneo yasiyo rasmi kama kwenye mabonde.


“Sisi kama kata tunaenda kuunda kikosi kazi ambacho kitafanya kazi kuanzia ngazi ya mtaa ,kitahusu mazingira na afya,tutaoa elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira na kisha tutaanza kuchukulia hatua wananchi ambao watakiuka sheria nakutupa taka hovyo kwenye mabonde na mitaani,tutakuwa na walinzi kwenye haya mabonde watafanya kazi usiku na mchana ,na ukionekana unatupa taka hovyo faini itahusika kwa mujibu wa sheria”.


Wadau mbalimbali ambao wameshiriki kuadhimisha siku hii ikiwemo taasisi ya SHIPO , Benki ya Taifa ya Uchumi (NBC),wanafunzi pamoja na vikundi vya vijana vinavyojishughulisha na mazingira ,wamesema jamii inatakiwa kutambua kuwa taka ni mali hivyo wanaweza kuzikusanya kwa utaratibu wakuzitenga taka ngumu zisizooza kama vile chupa za plastiki na zikatumika kwenye utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.


Halmashauri ya Mji Njombe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira pamoja na wananchi imeungana na nchi mbalimbali Duniani kuadhimisha siku ya usafishaji duniani kwa kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya Mji wa Njombe .

New Posts

Libya yatangaza hali ya dharura ya mwaka mzima baada ya mafuriko

  Serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura ya mwaka mzima kwa shabaha ya kuzuia kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokuumbw...