Friday, January 6, 2017

Jerry Muro aipigia magoti TFF


MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ameomba msamaha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) asamehewa adhabu ya mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka.

Julai mwaka jana, Muro alifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. milioni 3 baada ya kukutwa na hatia katika mashtaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF dhidi yake.

Katika barua yake kwa TFF, Muro amesema kwamba anakiri kupata barua ya kufungiwa kutoka Kamati ya Maadili, lakini anaomba msamaha baada ya kutumikia nusu ya adhabu yake.

Muro ameomba apunguziwe adhabu na kurudi kutekeleza majukumu yake kwa mwajiri wake Yanga kuanzia kipindi hiki cha michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayoendelea visiwani Zanzibar.

Mapema wiki iliyopita, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa mahasimu, Simba, Hajji Manara alimwombea msamaha Muro.
Aidha, wasemaji wa timu nyingine akiwemo Massau Bwire wa Ruvu Shooting walimwombea msamaha pia mwenzao huyo, wakiamini atakuwa amejirekebisha.

Muro alifungiwa Julai 8 mwaka jana baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam.

Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.

Kwa kosa hilo akahukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja wakati shtaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.

Katika shtaka hilo, Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shtaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya televisheni.

No comments:

Post a Comment

New Posts

Libya yatangaza hali ya dharura ya mwaka mzima baada ya mafuriko

  Serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura ya mwaka mzima kwa shabaha ya kuzuia kuenea magonjwa ya kuambukiza katika maeneo yaliyokuumbw...