Wednesday, March 1, 2017

Yanga yaipiga Ruvu Shooting 2 - 0




YANGA SC imerejesha matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 52 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukamata nafasi ya pili, nyuma ya vinara Simba SC wenye pointi mbili zaidi ingawa nao wamecheza mara 23.

Yanga iliyopoteza mechi ya tatu msimu huu Jumamosi baada ya kufungwa 2-1 na mahasimu Simba Uwanja wa Taifa, leo wangeweza kuvuna mabao zaidi kama si maamuzi ya utata ya marefa.

Yanga ilimaliza dakika 45 ikiwa pungufu, baada ya mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa kuonyeshwa kadi mbili za njano za utata ndani ya dakika mbili na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 45.

Chirwa alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 44 baada ya kuifungia Yanga bao safi ambalo lingekuwa la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Hassan Kessy, lakini refa Ahmada Simba wa Kagera akalikataa na kumuonyesha kadi ya njano.

Na Mzambia huyo akaonyeshwa kadi ya pili njano dakika ya 45 baada ya kuudunda mpira chini na kutolewa kwa kadi nyekundu.

Mapema dakika ya 31 Chirwa alifumua shuti kali langoni mwa Ruvu, ambalo lilimbabatiza mkononi beki Damas Makwaiya na Simba akaamuru mkwaju wa penalti, uliotiwa nyavuni na Simon Msuva kuipatia Yanga bao la kwanza.

Kipindi cha pili, Ruvu Shooting walianza kwa kuimarisha safu yao ya ushambuliaji, Fully Maganga akienda kuchukua nafasi ya Issa Kanduru na Yanga wakionekana kurejea kulinda ushindi.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga bao dakika ya 47 akiwa kweli ameotea na mwamuzi akalikataa bao hilo.

Deus Kaseke akamtangulizia pasi nzuri Msuva dakika ya 51, lakini kinara huyo wa mabao Ligi Kuu msimu huu akapiga shuti kali lililookolewa na beki mmoja wa Ruvu na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.

Emmanuel Martin akaifungia yanga bao la pili dakika ya nne ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida akimalizia kwa kichwa krosi ya Simon Msuva kutoka upande wa kulia.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Justine Zulu/Juma Mahadhi dk78, Simoni Msuva, Deus Kaseke/Emmanuel Martin dk78, Amisi Tambwe, Obrey Chirwa na Geoffrey Mwashiuya/Juma Said ‘Makapu’ dk63.

Ruvu Shooting; Bidii Hussein, Yussuf Nguya, Baraka Mtuwi, Damas Makwaiya, Said Madega, Kassim Dabi, Jabir Aziz, Shaaban Kisiga, Issa Kanduru/Fully Maganga dk46, Chande Magoja/Shaaban Msala dk49 na Abrahman Mussa.


No comments:

Post a Comment

New Posts

IJUE SCANIA P380[Mende]

Scania P380 Mende ni nini? Scania P380 ni mojawapo ya malori maarufu yaliyoundwa kwa nguvu na ufanisi wa hali ya juu, hasa kwa mazingira ya ...