DAKTARI Prudence Kiwia kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) amesema pombe na sigara si vyanzo vya saratani; wengi wanaougua hawakuwahi kutumia vilevi hivyo.
Amesema saratani zinazoongoza kila mwaka ni za shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake na tezi dume kwa wanaume, hivyo jamii inatakiwa iwe na tabia ya kufanya uchunguzi kila wakati.
Dk. Kiwia alisema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali na mashine kutoka Taasisi ya Jema Foundation iliyotembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuwafariji wagonjwa.
"Tumefurahi sana tumepokea misaada mingi kwa wagonjwa wetu, lakini kubwa ningependa kusisitiza wananchi kwa ujumla kwa sababu saratani ni hatari sana na njia bora ya kujikinga na saratani ni kufanya uchunguzi.
"Visababishi vingi vya saratani havionekani, wengi wanaongelea pombe na sigara, lakini si anayevuta sigara na kunywa pombe ndiye anaishia kupata saratani, hapana! Tuna wagonjwa wengi wanapata saratani, hawajawahi kutumia (sigara au pombe) alisema Dk. Kiwia.
Aliwataka wananchi kufanya uchunguzi mapema wanapoona mabadiliko yoyote kama vile uvimbe au kupata uchafu sehemu za siri.
"Kwa mwaka tunapata wagonjwa wengi sana, hasa shingo ya kizazi, maziwa kwa wanawake na kwa wanaume tezi dume, hao ni wengi sana, siwezi kukupa hata mfano kulinganisha na saratani zingine kama mfumo wa chakula, kichwa... ni wachache sana," alisema.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jema Foundation, Jema Baruan, alisema alikuwa mgonjwa wa saratani na alipona miaka minane iliyopita, na kwamba aligundulika kuwa na maradhi ya saratani ya mitoki inayoadhimishwa kila mwaka Septemba 15.
Alisema wameamua kuwatembelea wagonjwa wenye saratani ili kuwapa faraja na matumaini na pia wamewapelekea baadhi ya mahitaji yakiwamo magongo, viti vya wagonjwa, mashine ya sukari, mashine ya kupima mapigo ya moyo (BP) na vitu vingine.
"Nimepitia hivi, ninamshukuru Mungu nimeweza kuikabili saratani ya mitoki na nimepona, lakini yupo mwingine ambaye anapambana na ni Mtanzania kama mimi, nikaona si haba na yeye tuje tumguse kwa sababu matendo ya huruma ndiyo matendo yanayompendekeza Mungu.
"Asilimia kubwa hawaponi lakini kuna asilimia ndogo iliyobakia wanapona, mimi nilifanya tiba ya chemotherapy ambayo ilikuwa na mizunguko 16, sikuacha tiba katikati, nilikuwa nakula ipasavyo unakuta mtu anafanya tiba, lakini hali chakula ipasavyo, tiba inamzidia," alisema Baruan.
Alisema mgonjwa anatakiwa ale vizuri na kufanya mazoezi pamoja na kusikiliza ushauri wa daktari, akionya kuchanganya huduma za hospitalini tiba za kienyeji.
"Mimi nilijikita kwenye tiba niliyoambiwa, nikafanya mazoezi, nikala vizuri nilikuwa ninajilazimisha kula, changamoto ilikuwa kwenye kula, mgonjwa unatakiwa ujilazimishe kula, bahati nzuri nimepona," alisema.
Mwakilishi wa Kampuni ya Big Bon, Ahmed Salum alisema wagonjwa wa saratani wanateseka, hivyo wameona kuwachangia chochote kwa kuwaonesha upendo.
No comments:
Post a Comment